ZIARA YA HESHIMA KWA BANDA LA TANZANIA - FRUIT LOGISTICA, BERLIN, UJERUMANI – 6 FEBRUARI 2025

Mhe. Hassani Iddi Mwamweta, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani (ambaye pia anawakilisha Tanzania katika Uswisi, Jamhuri ya Czech, Slovakia, Romania, Poland, Hungary, Bulgaria, na Vatican), alitembelea banda la Tanzania kwenye maonesho ya kimataifa ya Fruit Logistica nchini Ujerumani. Balozi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, kuaminika kwa Tanzania kwenye soko la dunia, na kujenga mazingira rafiki kwa biashara. “Biashara ya Ulaya si rahisi, tunahitaji mipango madhubuti na ushirikiano thabiti,” alisema Balozi, akihimiza washiriki kujitengenezea fursa, kushirikiana na kujifunza kutoka kwa wadau wa kimataifa.
Balozi alipongeza Wizara ya Kilimo kupitia COPRA na shirikisho la TAHA kwa juhudi zao za kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, hatua muhimu kwa maendeleo ya soko la kimataifa. Balozi alifurahishwa kuona vijana wakishiriki katika maonesho haya. Moja wa wanufaika wa programu ya BBT, Bi. Asia Msuya, alipata nafasi ya kuzungumza na Balozi na kwa ujasiri akasema: “Nafanya kile ninachokipenda, bila aibu!” Hili ni ishara kuwa kizazi kipya kipo tayari kuleta mapinduzi kwenye sekta ya nafaka na mazao mchanganyiko (Februari 2025)