COPRA YAWANOA VIJANA WA BBT UGANI KUIMARISHA KILIMO CHA PARACHICHI
Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imeendesha mafunzo elekezi kwa vijana wa Programu ya Jenga Kesho Iliyobora Bora (BBT- Ugani) kwa kuwaandaa kushirikiana na wakulima wa parachichi ili kuboresha uzalishaji wa zao hilo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika mjini Iringa, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA Bi. Irene M. Mlola amewataka vijana hao kuzingatia maelekezo ya wakufunzi ili wapate maarifa yatakayowasaidia kutekeleza majukumu yao wanapokuwa na wakulima mashambani.
Mkurugenzi Mkuu Mlola amebainisha kuwa COPRA ni taasisi inayozingatia matokeo chanya ya kazi na kwamba vijana hao watapimwa kwa matokeo ya kazi zao, hivyo kila mmoja atumie elimu, ujuzi na maarifa yake kutekeleza wajibu wake huku akiwahakikishia kuwa watapatiwa vitendea kazi kwa mujibu wa mahitaji yao.
Aidha, Bi. Mlola amewatakia washiriki utekelezaji mwema wa majukumu akiwasisitiza kuzingatia sheria, taratibu na maadili ya utumishi wa umma na kuwahudumia wakulima kwa uadilifu, uaminifu na weledi wa hali ya juu.
Kwa upande wake Mkuu wa Sehemu ya Mazao ya Bustani na Pareto, Bi. Lilian Mpinga amesema kuwa mafunzo hayo yanayofanyika yamewakutanisha vijana 50 wahitimu wa shahada za kilimo waliopatikana kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) watapatiwa mafunzo ya utumishi wa umma na namna ya kusimamia kilimo cha parachichi na watasambazwa kwenye maeneo yanayolima parachichi nchini.
Nao washiriki wa mafunzo hayo kwa nyakati tofauti wameahidi kutumia ujuzi wao kujifunza kwa bidii na kuwa chachu ya maendeleo ya uzalishaji wa zao la parachichi.
