COPRA YACHANGIA UZALISHAJI WA MBEGU BORA MUHEZA
Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imegawa jumla ya kilo 300 za mbegu mama ya zao la mbaazi kwa wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, kwa lengo la kuchochea uzalishaji wa mbegu bora na kuongeza tija kwa wakulima wa zao hilo.
Mbegu hizo zitatumika katika uzalishaji unaofanyika kwenye kata tano ambazo ni Kang’ata, Mazingara, Mkata, Kitumbi na Ndolwa, katika eneo lenye jumla ya ekari 76. Katika mpango huu, wakulima 12 waliotambuliwa watashiriki moja kwa moja katika uzalishaji wa mbegu, huku mbegu zitakazozalishwa zikitarajiwa kunufaisha zaidi ya wakulima 500 katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na maeneo jirani.
Kupitia mpango huo, inatarajiwa kuzalishwa takribani tani 90 za mbegu bora za mbaazi zitakazosaidia kuboresha upatikanaji wa mbegu zenye ubora na kuimarisha uzalishaji endelevu wa zao hilo.
Utekelezaji wa mradi huu unahusisha ushirikiano wa wadau mbalimbali muhimu ikiwemo COPRA iliyochangia kwa kutoa mbegu za mtaji na itazinunua mbegu zitakazozalishwa, huku Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ikisimamia shughuli zote za uzalishaji. Wakulima watatumia mashamba yao kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu, wakati Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) ukitoa elimu na miongozo ya uzalishaji wa mbegu bora. Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) itahakikisha ubora wa mbegu zinazozalishwa kwa kuzipima na kuzithibitisha kabla ya matumizi.
Hatua hii ya COPRA inaelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za Serikali na wadau wake katika kuimarisha sekta ya kilimo hususan katika kuongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima na kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa jamii zinazotegemea kilimo.
