Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Cereals and Other Produce Regulatory Authority

(COPRA)

COPRA Logo
"Commercialization of the Tanzania’s Food systems to catalyze growth and resilience"

COPRA YAKABIDHI TANI 12 ZA MBEGU BORA ZA UFUTA, CHOROKO NA MBAAZI

Reason Image

Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), imekabidhi jumla ya tani 12 za mbegu bora za ufuta, choroko na mbaazi kwa uongozi wa Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kugawiwa bure kwa wakulima wa mkoa huo.

 

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mbegu hizo , Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,Mhe. Kanali Patrick Sawala ameipongeza Wizara ya Kilimo kupitia COPRA kwa hatua ya kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora bila gharama, na kubainisha kuwa mkoa wa Mtwara umekabidhiwa tani 6 za mbegu ya ufuta, tani 3 za mbegu ya choroko na tani 3 ya mbegu ya mbaazi.

 

Kanali Sawala ameongeza kuwa hatua ya kugawa mbegu bora bure kwa wakulima itapunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija kwa wakulima wanaojihusisha na mazao mchanganyiko katika mkoa huo.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Bi. Irene Mlola, amesema mamlaka hiyo imeamua kushirikiana na wakulima kuanzia hatua za awali za uzalishaji na kuhakikisha anapata mbegu bora kuanzia shambani, sambamba na kutoa mafunzo kwa maafisa ugani watakaosimamia uzalishaji wa mazao hayo.

 

"Tumeona tusikutane na mkulima sokoni pekee, bali tusimame naye bega kwa bega shambani ili kuhakikisha ubora unaanzia kwenye uzalishaji,” amesema Bi. Mlola.

 

Wakulima pamoja na maafisa ugani waliohudhuria hafla hiyo wameishukuru COPRA kwa hatua hiyo, wakisema itawasaidia kuongeza uzalishaji na kuboresha vipato vya wakulima.