Tarehe 17 Januari 2025, Mamlaka kwa kushirikiana na Mtandao wa Wadau wa Mazao ya Mikunde Tanzania (Tanzania Pulses Network – TPN), ilifanya kikao jijini Dar es Salaam na wanunuzi na wasafiris

Tarehe 17 Januari 2025, Mamlaka ya Udhibiti Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kwa kushirikiana na Mtandao wa Wadau wa Mazao ya Mikunde Tanzania (Tanzania Pulses Network – TPN), ilifanya kikao jijini Dar es Salaam na wanunuzi na wasafirishaji wa mazao nje ya nchi kutoka katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mikunde.
Lengo la kikao ni kupitia rasimu za kanuni za utekelezaji wa Sheria ya Usalama wa Chakula Sura 249 na marekebisho yaliyofanywa kupitia Sheria ya Nafaka na Mazao Mengine Sura 274. Sekta ya mikunde ina nafasi kubwa ya kuchangia ukuaji wa kilimo na uchumi wa Tanzania, hasa kupitia ongezeko la mapato yatokanayo na mauzo ya nje. COPRA imejipanga kuimarisha mifumo ya masoko na kuwezesha biashara ili kufungua fursa kubwa katika sekta mazao ya mikunde. Mahitaji ya mazao ya mikunde duniani yanaendelea kuongezeka kutokana na faida zake za lishe na mchango wake katika kilimo endelevu.
Tanzania, ikiwa mzalishaji wa pili wa mazao ya mikunde kwa ujumla, ina nafasi kubwa ya kunufaika na mwenendo huu. Tathmini inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya mikunde nchini Tanzania unatarajiwa kuongezeka kutoka tani milioni 1.71 mwaka 2023 hadi tani milioni 1.77 ifikapo 2028, ongezeko linalochangiwa na wakulima wadogo wanaotegemea mazao hayo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na biashara.