TANZANIA NA DRC KUIMARISHA FURSA ZA BIASHARA YA MAZAO
Tanzania inaendelea kupanua biashara ya mazao ya chakula katika nchi jirani, huku Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) ikiimarisha mifumo rasmi ya biashara na kufungua fursa zaidi kwa wakulima na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
Katika kikao kilichokutanisha viongozi wa sekta ya kilimo na ujumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ulioongozwa na mshauri wa Rais wa nchi hiyo katika masuala ya Uchumi na Uwekezaji, Bw. Tony Bandio Munongo, Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara katika mazao ya chakula, masoko na usafirishaji.
Alieleza kuwa hatua hiyo inaunga mkono maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuzalisha chakula cha kutosha na ziada ili kulisha kibiashara nchi za ukanda wa EAC na SADC.
Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Bi. Irene Mlola alishiriki kikao hicho pamoja na viongozi wa taasisi nyingine za Serikali na wadau wa sekta ya kilimo.
Kupitia juhudi hizi, COPRA inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi kujisajili kupitia mfumo wa COPRA MIS na kurasimisha biashara zao za mazao hapa nchini, hatua itakayochochea uwazi wa biashara, upatikanaji wa taarifa za masoko na ushindani wenye tija katika soko la kikanda na kimataifa.
Hatua hizi zinaendelea kuiweka Tanzania kama kitovu cha biashara ya mazao ya chakula katika Afrika Mashariki na Kati.
