COPRA YAGAWA MBEGU BORA YA MBAAZI MANYARA
Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imeanza mwaka 2026 kwa kukabidhi tani 2.7 za mbegu bora ya mbaazi aina ya Mali kwa Mkoa wa Manyara kwa ajili ya kugawiwa kwa wakulima. Mbegu hizo zimekabidhiwa kwa Katibu Tawala wa mkoa huo, Bi. Mariam Muhaji ikiwa ni sehemu ya mchango wa COPRA katika kuendeleza uzalishaji wa mazao ya kimkakati nchini.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Kaimu Mkuu wa Kanda ya Kati wa COPRA Bw. Andrew Mgaya, amesema mgao huo ni sehemu ya asilimia 60 ya mapato ya mauzo ya mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani katika mwaka wa fedha 2024/2025 yaliyotengwa mahsusi kwa ajili ya uendelezaji wa mazao huku akibainisha kuwa katika awamu hii mikoa ya Singida na Dodoma itanufaika.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bi. Mariam Muhaji, ameishukuru COPRA kwa kurejesha kwa uaminifu sehemu ya faida ya mfumo wa stakabadhi ghalani na kuwataka wakulima kuendelea kutumia mfumo huo. Ameeleza kuwa katika msimu uliopita mkoa uliuza tani 73,777 za mbaazi kupitia mfumo huo jambo lililowezesha kupatikana kwa mgao huu wa mbegu.
Ameongeza kuwa mbegu hizo zitagawiwa katika halmashauri tatu za Mkoa wa Manyara ambapo Babati itapokea tani 1.2, Kiteto tani 1 na Hanang nusu tani. Kwa msingi huo, COPRA inaendelea kuhimiza wakulima wa mbaazi na mazao mengine kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani kama njia salama yenye tija na yenye faida katika masoko ya mazao.
