COPRA YAGAWA TANI 2.6 YA MBEGU ZA MBAAZI SIMIYU
Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imeendelea kutekeleza jukumu lake la kusimamia na kuendeleza masoko ya mazao kwa kutoa Tani 2.6 za mbegu ya zao la mbaazi kwa wakulima wa Mkoa wa Simiyu, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushiriki wa wakulima katika mfumo wa kuuza mazao kidijitali.
Mbegu hizo zimekabidhiwa rasmi kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha na Meneja wa COPRA Kanda ya Ziwa Bw. Said Mambo kwa ajili ya kusambazwa katika wilaya tano za Mkoa wa Simiyu na kugawiwa kwa wakulima wa zao la mbaazi.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano Mhe. Macha amesisitiza kuwa mbegu hizo ni mahsusi kwa wakulima wanaouza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani. Ameeleza kuwa mfumo huo una mchango mkubwa katika kuhakikisha wakulima wanapata bei yenye tija, masoko ya uhakika na usalama wa mazao yao.
Aidha, Mhe. Macha ameipongeza COPRA kwa juhudi zake endelevu za kuhamasisha wakulima kutumia mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuinua uchumi wa wakulima na kukuza sekta ya kilimo mkoani Simiyu.
