Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Cereals and Other Produce Regulatory Authority

(COPRA)

COPRA Logo
"Commercialization of the Tanzania’s Food systems to catalyze growth and resilience"

COPRA YAWAFIKIA KATAVI MBEGU ZA UFUTA NA MBAAZI

Reason Image

Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imeendelea kuonesha mchango wake muhimu katika kukuza kilimo biashara kwa kugawa mbegu bora za ufuta (kilo 2,500) na mbaazi (kilo 500) kwa wakulima wa mkoa wa Katavi hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, tija na kipato cha wakulima.

Akipokea mbegu hizo Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko amewataka wakulima kutumia mbegu hizo kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kuzitumia kinyume na taratibu ikiwemo kuziuza na kusisitiza kuwa serikali imewekeza kupitia COPRA ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo bora zitakazosaidia kuongeza mavuno na kuimarisha uchumi wa kaya.

Naye Mkuu wa Kanda ya Magharibi Laison Gilbert Nzunda amesema kuwa Mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto za upatikanaji wa mbegu bora na kusimamia ubora wa mazao Pamoja na kuweka mazingira rafiki ya soko kwa wakulima.

Nzunda amesisitiza kuwa jukumu la COPRA si udhibiti pekee bali pia ni kuchochea uzalishaji na thamani ya mazao mchanganyiko ikiwemo ufuta, mbaazi na mazao mengine ya kimkakati.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi upande wa Uchumi na Uzalishaji, Nehemia James amesema kuwa halmashauri zote za mkoa wa Katavi zina wajibu wa kusimamia kwa karibu zoezi la usambazaji wa mbegu hizo ili kuwafikia wakulima halisi wanaolima ufuta na mbaazi ili kuepusha upotevu na kuhakikisha dhamira ya serikali inafikiwa.

Ugawaji wa mbegu za ufuta na mbaazi mkoani Katavi ni sehemu ya mkakati mpana wa COPRA kuhakikisha mkoa huo unatumia kikamilifu fursa ya ardhi yake kubwa na rutuba huku wakulima wakihamasishwa kuzalisha kwa tija na kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.